
Licha ya kwamba tumekuwa tukichukulia kwamba fedha mara nyingi inaweza kumfanya mtu akawa na furaha katika maisha yake lakini wakati huohuo wapo ambao fedha walizonazo zinawaweka katika mazingira magumu na kujikuta wakikufuru kwa kusema Mungu asingewajaalia kuwa nazo.
Wengi wetu tumezoea kuona ndoa zikivunjika kutokana na umaskini wa wanaume lakini kwa taarifa yako zipo pia ambazo zimevunjika kwa sababu ya utajiri.
Katika utafiti ambao nimeufanya, watu wengi sana wanaotaka kuoa hupenda kuangalia kwanza familia anayotoka yule anayetaka kufunga naye ndoa.
Baadhi hawapendi kuolewa ama kuoa mtu ambaye ni tajiri wakitoa sababu ya kwamba, wenye nazo wakati mwingine wanakuwa na manyanyaso sana.
Ninachofahamu mimi ni kwamba, siyo wote wenye tabia hiyo lakini wapo ambao kweli hutumia fedha zao kufanya lolote wanalotaka kwa wenza wao bila kujali kama linaweza kuudhi ama kufurahisha.
Ni katika mazingira hayo ndipo tunaweza kuona jinsi gani pia fedha inaweza kujenga ama kubomoa ndoa. Fedha ni mhimili muhimu sana katika ndoa.
Siwezi kusema bila pesa hakuna ndoa kwani wapo maskini wanaooana na wanakuwa na maisha mazuri tu lakini kiuhalisia ndoa inanoga zaidi pale ambapo mahitaji muhimu katika maisha yenu yanapopatikana.
Hata hivyo, ukijaribu kufuatilia utagundua kwamba ni wanawake wachache sana ambao wameolewa na wanaume wenye nazo na wanayafurahia maisha. Wapo ambao wanapata kila wanachokitaka lakini bado wanakuwa katika maisha ya huzuni na machafuko kila siku.
Watu wa pembeni wakiwaona wanadhani wanafurahia maisha yao kwa kupata kila kitu kumbe wao wenyewe wanajuta huku mawazo ya kutoka nje ya ndoa yakiwajia kila mara.
Machafuko ndani ya ndoa yanakuja kama upendo baina ya wanandoa utakosekana. Hata mkiwa matajiri lakini kama hakuna upendo ndoa haiwezi kudumu.
Pesa inachukuliwa kama chanzo cha maovu yote hasa kama zimedondokea kwa mtu limbukeni asiyejua maisha ni nini!
Wapo ambao wanapojaaliwa kuwa nazo hufanya mambo ambayo yanaweza kuwachukiza wenza wao. Ni wanaume wangapi hutumia pesa zao kulewea kiasi cha kusababisha vurugu ndani ya nyumba?
Nasema hivyo kwa sababu baadhi ya watu wamekuwa wakitumia pesa kunywea pombe na kuwafanya matusi, kupigana na kutenda mambo ambayo kimsingi hayawezi kumfurahisha mke aliyestaarabika kuwa sehemu ya maisha yao.
Si hivyo tu, kuna wanaume ambao fedha zao zinawasukuma kuendekeza starehe kiasi cha kuwafanya wasahau kufanya mambo ya msingi.
Wanawake wengi sana wamekuwa wakitoa malalamiko yao kwamba waume zao wamekuwa wakibadilika kitabia kadiri vipato vyao vinavyoongezeka.
Kuna ambao walikuwa hawajui baa wala kumbi za starehe ziliko pindi kipato chao kilipokuwa kidogo lakini baada ya kuzinasa hujikuta wakiwa walevi kupindukia na wanaolala katika kumbi za starehe huku wakiwa na vimada, hali ambayo sidhani kama yupo mwanamke anayeweza kuvumilia.
Niseme tu kwamba, wewe msichana ambaye umeolewa na mume tajiri limbukeni pole ila tahadhari ni kwa wale ambao wanatafuta wachumba.
Usikimbilie kuolewa na mwanaume ambaye ni tajiri bila kumsoma vizuri. Kumbuka wapo walioshawishiwa kwa mali na fedha wakaingia kwenye ndoa lakini sasa hivi wanatamani kutoka lakini wanashindwa.
Wanatamani kutoka kwa kuwa hawapati yale mapenzi waliyotarajia badala yake wananyanyaswa, wanadharauliwa na kusalitiwa kila kukicha. Usiingie huko, fanya maamuzi sahihi!