
Wiki hii nataka kuzungumzia huu ugonjwa hatari wa Ukimwi ambao baadhi yetu tunauchukulia poa na matokeo yake tunajiweka katika mazingira hatarishi ikiwa ni pamoja na baadhi ya watu kugeuza miili yao kuwa biashara ya kujipatia kipato.
Ndugu zangu, kusema ukweli hali inatisha na sidhani kama tukiendelea hivi tunaweza kutimiza malengo yetu ya kupunguza kasi ya maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi na ikiwezekana kuutokomeza kabisa ugonjwa huo hatari.
Kila siku tunashuhudia watu wanakufa kwa maradhi hayo, tunawaona walioathirika wakiwa majumbani au hospitali wakiteseka huku wakikosa matumaini ya kuiona kesho.
Cha ajabu wala hatushtuki, tunaona ni jambo la kawaida tu na matokeo yake tunaendelea na tabia ambazo mwisho wake zinaweza kutufanya tukawa miongoni mwa walioathirika.
Kuna watu wanaonekana kutojali maisha yao kabisa. Kubadili wapenzi imekuwa ni fasheni, leo yuko na huyu na kesho yuko na yule. Vibinti vidogo havioni hatari kutembea na watu wazima ambao wanaweza kuwaita baba zao, ukiwauliza wanakuambia maisha magumu, wanatafuta pesa ya kula! Hii ni hatari sana.
Mbaya zaidi wapo ambao wamegeuza mapenzi kama kitega uchumi na baadhi ya familia zimekubaliana na hali hiyo. Watoto wa kike usiku wanalazimishwa kwenda kujiuza ili walete pesa za matumizi nyumbani, jamani tunaenda wapi?
Juzi nilitembelea eneo moja maarufu kwa biashara ya ngono. Lipo pale Sinza Afrikasana. Kutokana na mwezi mtukufu hawakuwa wengi lakini wachache niliowaona walinisikitisha sana.
Nilikutana na vibinti vitatu. Maskini viliponiona vikadhani na mimi ni mteja, vikaanza kujinadi kwangu kila kimoja kikijisifia kwamba kiko bomba. Nilibaki nimepigwa butwaa, machozi yalinilengalenga huku nikishindwa kuamini nilichokiona mbele yangu.
Niliumia sana! Niliumia kwa kuwa baadhi yao walikuwa ni kama wadogo zangu. Nikajiuliza, hivi hawa hawana wazazi? Hawana ndugu? Inakuwaje wanafanya biashara hii hatari kwa maisha yao? Jibu nilikosa!
Wakati nikiwa nimeinamisha kichwa mara akapita kijana mmoja akiwa kwenye bodaboda na kuwauliza kwa kuwakebehi akijua mimi ni mteja na niko pale ‘kuopoa’. Alisema kwa sauti: ‘Nyie hamuogopi Ukimwi?’
Kwa swali lile nilitarajia wale wasichana wangeweza kutahayari ama hata kushtuka, lakini wala! Mbaya zaidi ni kwamba mmoja wao alitoa maneno yaliyonifanya nishangae.”Kwa raha zetu, Ukimwi utajiju. ”Ndivyo alivyojibu binti huyo.
Ndugu zangu, sikatai maisha ni magumu lakini ni kweli ugumu huo ndiyo ukufanye uugeuze mwili wako biashara? Kwanza unajidhalilisha lakini pia unajiweka katika mazingira hatari ya kuambikizwa maradhi ya zinaa na Ukimwi.
Mimi nadhani kuna kitu unaweza kukifanya badala ya kuamua kuugeuza mwili wako kitega uchumi.
Ni kweli kwa ulimwengu ulivyo sasa utapata wanaume wa kukupa kiasi chochote cha pesa ili uwauzie penzi lakini kumbuka unaiweka rehani kesho yako.