Stori: CHANDE ABDALLAH NA DENIS MTIMA KIBAO
kimegeuka! Yule mganga anayejitapa kumtengenezea nyota ya mvuto staa wa
Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’, Ustadh Yahya yamemkuta
mazito.
Habari
za uhakika zilizolifikia gazeti hili zinaeleza kuwa jamaa huyo
anahenyeshwa na polisi akiwa mahabusu kufuatia madai ya wizi wa gari
aina Toyota Rav 4 ‘milango mitatu’.
Kwa mujibu wa chanzo makini, gari hilo liliibwa wiki kadhaa maeneo ya Msimbazi-Kariakoo jijini Dar.
HABARI ZA AWALI Habari za awali zilidai kuwa
gari hilo lilifika mikononi mwa Ustadh kutoka kwa mwanamke aliyetajwa
kwa jina moja la Mwanahamis ambaye ilisemekana kwamba alikuwa akichukua
dawa kwa mganga huyo.
Ilidaiwa kuwa mwanamke huyo naye alihongwa gari hilo na mume wa mtu
huku akiwa hajui kuendesha hivyo aliliweka poni kwa Ustadh ambaye alimpa
dawa ambayo aliipeleka Kigoma kuwauzia watu wake.

Hata
hivyo, ilizidi kudaiwa kwamba mwanamke huyo alichukua dawa za shilingi
milioni 3 lakini akashindwa kurudisha fedha hizo na riba waliyokubaliana
na mganga huyo.
Ikazidi kudaiwa kuwa, Ustadh alimuongezea dawa
nyingine mwanamke huyo hadi kufikia deni la shilingi milioni 6 ndipo
akaamua kulichukua gari hilo.
NI UZEMBE?
Ukiacha stori hizo za awali ambazo zilikosa ‘balansi’, kuna habari
nyingine kuwa gari hilo mali ya Edric Magayane liliibwa baada ya kuachwa
eneo la tukio likiwa ‘sailensi’ bila mtu ndani.
Ilielezwa kwamba
aliyekuwa na gari hilo aliingia dukani kununua vitu na alipotoka
alichanganyikiwa akidhani gari hilo lilikuwa limevutwa na watu wa ‘breki
dauni’ waliokuwa wakivuta magari yaliyoegeshwa hovyo katikati ya jiji.
Habari zinasema kuwa mhusika alikwenda kulitafuta katika ‘yadi’ zinakopelekwa magari yaliyovutwa lakini hakuliona.
POLISI “Alichokifanya ni kwenda kuripoti polisi ambao walianza kulisaka Dar bila mafanikio.
“Wakati polisi wakiendelea kulisaka kuna mtu akasema amemuona Ustadh akitanua nalo.
“Yule mwenye gari (Magayane) alimtafuta Ustadh hakumpata. Akaelekezwa nyumbani kwake, Kigogo Luhanga, Dar au Urambo, Tabora.
“Jamaa alipatafuta nyumbani kwa Ustadh, Kigogo hadi akafika akiwa na polisi waliovalia kiraia lakini hawakumkuta.
ALITAKA KULIRUDISHA? “Waliambiwa amesafiri Tabora. Pia walihakikishiwa kwamba kweli Ustadh alikuwa na gari hilo. Jamaa akaambulia namba za simu.
“Alipompigia simu Ustadh alimwambia kama gari limeibwa ana uwezo wa
kutumia uganga wake kulirejesha kwa kuwa ni mtaalam wa mambo hayo.
“Ustadh aliomba apewe fedha ili afanye mambo yake gari lirudi. Kweli
alitumiwa fedha, lakini akawa anazungusha huku akijiita majina lukuki
kama Maimuna na mengine,” kilisema chanzo hicho cha kuaminika.
MKOKO WATAFUTIWA MTEJA
Baadaye polisi walifanya uchunguzi na kubaini kuwa, gari hilo lilikuwa
likitafutiwa mteja mkoani Tabora lakini ilishindikana kutokana na kukosa
‘dokyumenti’ muhimu.
GARI LAKAMATWA
Habari zilizidi kutiririka kwamba, wakati Ustadh akikatiza na gari hilo
Tabora mjini ndipo alipokamatwa na polisi kisha kuwekwa nyuma ya nondo
za mahabusu kabla ya kusafirishwa jijini Dar kwa hatua zaidi za
kisheria.
MASHITAKA MAWILI Habari za
uhakika zilieleza kuwa, Ustadh alipofikishwa Kituo cha Polisi cha Kati
(Central), Dar alifunguliwa mashitaka mawili; wizi wa gari na kujipatia
fedha kwa njia isiyo halali.
Baada ya kujikusanyia habari hizo, juzi
gazeti hili lilishuhudia polisi wakipekuwa nyumbani kwa Ustadh kisha
kumrejesha kituoni kwa ‘difenda’ huku amepigwa pingu mikononi.
MMILIKI ANENA Akizungumza na gazeti hili juzi, mmiliki wa gari hilo, Magayane alikiri maelezo yote juu ya habari hiyo.
Alipoombwa namba ya jalada la kesi aliitaja kuwa ni MS/RB/827/ 2014-WIZI WA GARI NA KUJIPATIA FEDHA KWA NJIA ISIYO HALALI.
Jitihada za gazeti hili kuzungumza na Ustadh juu ya msala huo mzito
ziligonga mwamba kwa kuwa simu yake ilikuwa haipatikani na bado alikuwa
mahabusu huku ikelezwa kwamba soo limemkalia vibaya.
DIAMOND KAINGIA MITINI?
Kwa mujibu wa chanzo kingine, Diamond amekuwa akiombwa kumsaidia jamaa
lakini akaingia mitini kwa madai kuwa hapendi kuhusishwa na Ustadh
ambaye aliahidi msanii huyo kupata majanga makubwa baada ya kumkimbia na
kwenda kwa waganga wengine.
Diamond alipotafutwa juzi kwa njia ya
simu hakupatikana huku mmoja wa watu wa timu yake akisema yupo Afrika
Kusini ‘Sauzi’ kwa ajili ya kufanya kolabo na D’Banj wa Nigeria.